Luke 15

Mfano Wa Kondoo Aliyepotea

(Mathayo 18:12-14)

1 aBasi watoza ushuru na wenye dhambi wote walikuwa wanakusanyika ili wapate kumsikiliza Isa. 2 bLakini Mafarisayo na walimu wa sheria wakanung’unika wakisema, “Huyu mtu anawakaribisha wenye dhambi na kula nao.”

3 cNdipo Isa akawaambia mfano huu: 4 d“Ikiwa mmoja wenu ana kondoo mia moja, naye akapoteza mmoja wao, je, hawaachi wale tisini na tisa nyikani na kwenda kumtafuta huyo aliyepotea mpaka ampate? 5Naye akishampata, humbeba mabegani mwake kwa furaha 6 ena kwenda nyumbani. Kisha huwaita rafiki zake na majirani, na kuwaambia, ‘Furahini pamoja nami; nimempata kondoo wangu aliyepotea.’ 7 fNawaambieni, vivyo hivyo kutakuwa na furaha zaidi mbinguni kwa sababu ya mwenye dhambi mmoja atubuye, kuliko kwa wenye haki tisini na tisa ambao hawana haja ya kutubu.”

Mfano Wa Sarafu Iliyopotea

8“Au ikiwa mwanamke ana sarafu za fedha kumi, naye akapoteza moja, je, hawashi taa na kufagia nyumba na kuitafuta kwa bidii mpaka aipate? 9 gNaye akiisha kuipata, huwaita rafiki zake na majirani na kuwaambia, ‘Furahini pamoja nami; nimeipata ile sarafu yangu ya fedha iliyopotea.’ 10 hVivyo hivyo, nawaambia, kuna furaha mbele ya malaika wa Mungu juu ya mwenye dhambi mmoja atubuye.”

Mfano Wa Mwana Mpotevu

11 iIsa akaendelea kusema: “Kulikuwa na mtu mmoja aliyekuwa na wana wawili. 12 jYule mdogo akamwambia baba yake, ‘Baba, nipe urithi wangu.’ Hivyo akawagawia wanawe mali yake.

13 k“Baada ya muda mfupi, yule mdogo akakusanya vitu vyote alivyokuwa navyo, akaenda nchi ya mbali, na huko akaitapanya mali yake kwa maisha ya anasa. 14Baada ya kutumia kila kitu alichokuwa nacho, kukawa na njaa kali katika nchi ile yote, naye akawa hana chochote. 15 lKwa hiyo akaenda akaajiriwa na mwenyeji mmoja wa nchi ile ambaye alimpeleka shambani kwake kulisha nguruwe. 16 mAkatamani kujishibisha kwa maganda waliyokula wale nguruwe, wala hakuna mtu aliyempa chochote.

17“Lakini alipozingatia moyoni mwake, akasema, ‘Ni watumishi wangapi walioajiriwa na baba yangu ambao wana chakula cha kuwatosha na kusaza, bali mimi hapa nakufa kwa njaa! 18 nNitaondoka na kurudi kwa baba yangu na kumwambia: Baba, nimetenda dhambi mbele za Mungu na mbele yako. 19Sistahili tena kuitwa mwanao; nifanye kama mmoja wa watumishi wako.’ 20 oBasi akaondoka, akaenda kwa baba yake.

“Lakini alipokuwa bado yuko mbali, baba yake akamwona, moyo wake ukajawa na huruma. Akamkimbilia mwanawe, akamkumbatia na kumbusu.

21 p“Yule mwana akamwambia baba yake, ‘Baba, nimekosa mbele za Mungu na mbele yako. Sistahili kuitwa mwanao tena.’

22 q“Lakini baba yake akawaambia watumishi, ‘Leteni upesi joho lililo bora sana, tieni pete kidoleni mwake na viatu miguuni mwake. 23Leteni ndama aliyenona, mkamchinje ili tuwe na karamu, tule na kufurahi. 24 rKwa maana huyu mwanangu alikuwa amekufa na sasa yu hai tena; alikuwa amepotea na sasa amepatikana!’ Nao wakaanza kufanya tafrija.

25“Wakati huo, yule mwana mkubwa alikuwa shambani. Alipokaribia nyumbani, akasikia sauti ya nyimbo na watu wakicheza. 26Akamwita mmoja wa watumishi na kumuuliza, ‘Kuna nini?’ 27Akamwambia, ‘Ndugu yako amekuja, naye baba yako amemchinjia ndama aliyenona kwa sababu mwanawe amerudi nyumbani akiwa salama na mzima.’

28 s“Yule mwana mkubwa akakasirika, akakataa kuingia ndani. Basi baba yake akatoka nje na kumsihi. 29Lakini yeye akamjibu baba yake, ‘Tazama! Miaka yote hii nimekutumikia na hata siku moja sijaacha kutii amri zako, lakini hujanipa hata mwana-mbuzi ili nifurahi na rafiki zangu. 30 tLakini huyu mwanao ambaye ametapanya mali yako kwa makahaba aliporudi nyumbani, wewe umemchinjia ndama aliyenona!’

31 u“Baba yake akamjibu, ‘Mwanangu, umekuwa nami siku zote na vyote nilivyo navyo ni vyako. 32 vLakini ilitubidi tufurahi na kushangilia kwa sababu huyu ndugu yako alikuwa amekufa na sasa yu hai; alikuwa amepotea naye amepatikana.’ ”
Copyright information for SwhKC